Zitto ahujumiwa
Na Sarah Mossi
MWENENDO wa kisiasa katika vyama vikuu vya kisiasa nchini, umekuwa ni wa kutilia shaka kutokana na kila chama kuendeleza ubarikio batili wa dhambi inayoviongezea majeraha badala ya kuyaponyesha.
Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikikabiliana na tofauti ya makundi kati ya wabunge wake ambao siku hizi wananyukana kwa maneno makali, upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nako hali si shwari.
Habari zilizolifikia Mtanzania kwa wiki kadhaa sasa, zinabainisha wazi kwamba ndani ya Chadema kunafuka moto unaoweza kuuitwa wa mazoea kwani umekuwa ukitumika kuwachoma zaidi viongozi wa chama hicho wanaotoka nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Hali hiyo katika vyama vya CCM na Chadema, inakikumba pia Chama cha Wananchi (CUF), na hasa baada ya tamko la Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad la kumtambua Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Baada ya tamko hilo la wiki iliyopita, baadhi ya wanachama wamezua mtafaruku mkubwa unaowalazimu viongozi wakuu wa chama hicho kuhaha huku na kule kutuliza mizuka ya wanachama wao ambao hawakufurahishwa na hatua hiyo, kiasi cha kuwatuhumu viongozi wao kwamba wamehongwa na SMZ.
Inaelezwa na wachambuzi wetu kuwa yaliyompata aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Walid Amani Kaborou ambaye harakati za kumuengua zilipangwa na kuiva, kabla ya kujikuta amezingirwa akaamua kurejea CCM, ambako alitunukiwa ubunge wa Afrika Mashariki, sasa yanamzingira Zitto.
Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kutokana na kujizolea umaarufu uliotokana na mtindo wa kampeni zake kwa kutumia helikopta katika kuusaka urais, kichwa kilimvimba akaanza kujihesabu kama shujaa wa Chadema.
Uwezo wa wabunge wa chama hicho hasa Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe (marehemu) na Dk. Wilbroad Slaa, ulikifanya chama hicho kuanza kuvutia wanachama wengi, na hasa rika la vijana, ingawa hatua hii ilibomoa umaarufu Mbowe siku hadi siku.
Mbowe na kundi lake linaloshirikisha baadhi ya wanasiasa walioingizwa ndani ya chama hicho kwa ushawishi wa Zitto walianza mkakati wa kumnyofoa Zitto katika madaraka ya chama.
Zitto alipoufahamu aliamua kujitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti katika uchaguzi uliopita na kwa mizengwe Mbowe akawa mgombea pekee bila ushindani.
Mzee Edwin Mtei aliasisi mango huo kumlinda Mbowe kwa kigezo cha ukabila na undugu (baba mkwe) na kuhakikisha chama kinabaki kumilikiwa na waliokianzisha, wenye asili ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Baada ya uchaguzi Mbowe alikubali kumuacha Zitto katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kwa lengo la kumhadaa Zitto na wafuasi wake ili waanze kushughulikiwa mmoja baada ya mwingine.
Sababu nyingine ya kumwacha Zitto ilikuwa ni kulihadaa kundi la aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Hayati Chacha Wangwe aliyefariki siku chache baada ya kuenguliwa katika wadhifa wake. Wangwe kama alivyo Zitto alikuwa akipinga matumizi makubwa ya fedha kwa viongozi wa makao makuu ya chama, na pia alikuwa akipinga tabia za ukabila na ubinafsi zilizojenga mizizi katika chama.
Kundi la Wangwe lilianza kumuunga mkono Zitto na inaelezwa kuwa Zitto alikuwa na mtaji mkubwa wa kumshinda Mbowe katika uchaguzi huo, lakini pia kundi la Mbowe nalo lilikuwa limejiandaa kuwa kama Zitto angeshinda, basi lisingekubali matokeo kutangazwa, kama ilivyofanyika kwa matokeo ya uchaguzi wa Baraza la Vijana la chama hicho.
Kikao kilichofanyika Dodoma hivi karibuni kikimshirikisha Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa (mbunge), Hemed Sabula, John Mrema, Erasto Tumbo, Benson Kigaila, Halima Mdee (mbunge), Lucy Owenya (mbunge) na Anna Komu (mbunge), kimeharibu mambo. Zitto mwenyewe alikuwa nje ya nchi.
Inaelezwa kuwa hiki kilikuwa moja ya harakati za kummaliza Zitto zinazofanywa kwa siri ndani chama hicho. Baadhi ya wanaotaka kumaliza Zitto kisiasa inaelezwa kuwa wanasiasa ambao amewaingiza Chadema kwa ushawishi wake, lakini wameungana na kundi la Mbowe na kuanza kumshambulia. Kundi hili linajumuisha wabunge wa viti maalum kama Susan Lyimo, aliyekuwa Chuo Kikuu Dar es Salaam sekta ya huduma za wanafunzi na alijiunga Chadema kwa ushawishi wa Zitto.
Mwingine ni Halima Mdee ambaye naye kama alivyo Lyimo, aliingizwa katika Serikali ya DARUSO kwa mgongo wa Zitto, na baadaye Chadema kabla hajapewa ubunge wa Viti Maalum, ubunge uliolalamikiwa kuwa ulitolewa kwa misingi ya ukanda na ukabila. Katika msingi huo huo, Zitto naye alifanikisha kuwepo kwa Mbunge Viti Maalum kutoka Kigoma aitwaye Mhonga Ruhwanya ambaye naye alihitimu Chuo Kikuu Dar es Salaam na huko hakuwa na nafasi yenye jina katika uongozi wa wanafunzi.
Ukiacha kundi hilo, lipo kundi la vijana kama John Mnyika na John Mrema ambao nao wamekuwa na mahusiano ya karibu na Zitto kabla ya kufahamiana na Mbowe. Hawa wote sasa hivi wanaimba wimbo wa Mbowe na walimpinga Zitto hadharani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa chama hicho. Sababu ya vijana hawa kumpinga Zitto ni ukaribu wa kikabila walionao kwa Mbowe na maslahi yao ya kimaisha.
Kwa upande wa watu wanaoonekana kuwapo kwenye kundi la kumuunga mkono Zitto na wanaonja joto ya jiwe ni Ofisa Habari wa chama hicho, David Kafulila ambaye katika kikao cha juzi cha Dodoma vyanzo vya habari zilisema Mbowe aliwasilisha hoja ya kutaka kufukuzwa uanachama wake. Wengine wanaotajwa kukumbwa na fagio la Mbowe ni mama mzazi wa Zitto ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Danda Juju ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa Chadema.
Vyanzo vya habari vimeiambia Mtanzania kwamba Kafulila anaponzwa na msimamo wake wa kutojua kupindisha maneno na kutokubali kuwa mtumwa kwa ajili ya maslahi ya wachache.
“Haya ni matatizo ya muda mrefu, Kafulila ni tatizo kwa maslahi yao kimsingi, lakini si ya chama, hajui kupindisha maneno na tupo hapa kujenga chama na mara nyingi ukweli unachukuliwa vibaya. Obama aliwahi kusema anapenda kukaa na wapinzani wake ili ajue wanamsaidiaje,” kilisema chanzo chetu.
Habari ambazo Mtanzania imezipata wakati tunakwenda mitamboni zilisema juzi kulikuwa na harakati za kufanyika kikao cha faragha kilichoitishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa kikiwahusisha wakurugenzi wote wa chama hicho. Kikao hicho kilikuwa na agenda ya kumhoji Kafulila juu ya kile kilichoandikwa kwenye magazeti na hatimaye kumtimua uanachama.
Habari za uhakika zilizotufikia zinasema kuwa Kafulila anapatiwa barua ya kutimuliwa leo. Kafulila alipoulizwa na Mtanzania, alisema: “Nakipenda sana chama changu na namheshimu Dk. Slaa… najua tatizo la msingi halijapatiwa dawa,” alisema Kafulila na kuongeza kuwa ameitwa na wazee wa Kigoma kuzungumza naye jana.
Mtanzania ilipozungumza na Zitto ambaye yuko nchini Ujerumani kwa sasa, alisema hatua yoyote ya kumfukuza mtu yeyote kwenye chama chao haitasaidia na kusisitiza kuwa chama chao hakihitaji migogoro kwa sasa.
Zitto alisema hatua yoyote itakayochukuliwa na kuonekana Kafulila kaonewa itakiweka chama chao pabaya na kuonya kuwa iwapo kikao kilichofanyika Dodoma kilikuwa cha kuwajadili watu kilikuwa ni cha makosa.
“Kipindi hiki wenzetu CCM wanagombana ilikuwa sisi tukijenge chama chetu na si kuonyosheana vidole. Ikumbukwe Kafulila ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, aligombea Uenyekiti wa Vijana Taifa na matokeo hayakutangazwa ingawa naamini alishinda.
“Katika chama chetu kila mmoja ana mchango wake katika kukipeleka chama mbele na makundi ya uchaguzi yaliisha mara baaada ya uchaguzi. Kuwaondoa hawa si vizuri lakini naamini Katibu Mkuu atayasawazisha haya,” alisema Zitto katika mahojiano ya simu.
Ukiacha mazungumzo hayo na Zitto, tayari Katibu Mkuu wa Chadema alikaririwa na vyombo vya habari wiki hii akipinga kuwepo kwa taarifa za kuwatimua wanachama. Kauli za Slaa hazina tofauti na zile ambazo amekuwa akitoa siku kabla ya uchaguzi hasa katika msimamo wake wa kutaka nafasi ya Katibu Mkuu ambapo awali alipinga kuitaka nafasi hiyo, lakini mwishoni aliikubali.
Kuna maelezo kuwa, mkakati wa Mbowe kutaka ubunge una lengo la kurejesha nguvu ya kisiasa jukwaani ambayo ameipoteza miaka mitano inayomalizika. Lengo hilo likitimia anaamini kuwa atakuwa mgombea bora wa urais kwa mwaka 2015.
Dk. Slaa na Mbowe wamekuwa pamoja katika mambo kadhaa na umoja wao kwa sasa ni dhahiri kuwa una lengo la kumdhohofisha Zitto. Zitto anaelezwa kutumia kipindi cha yeye kutimuliwa katika Bunge mwaka juzi kujijengea umaarufu, hali iliyompa fursa mbalimbali ndani na nje ya chama hicho. Hili lilimkera Mbowe.
Kambi ya Mbowe inahofu kuwa Zitto alihitaji nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema kwa lengo la kujijenga heshima awanie urais mwaka 2015. Fursa ya 2015 ndiyo anayoitafuta Mbowe pia.
Kwa vyovyote vile, uhasama wa kambi hizi mbili ndani ya Chadema hauwezi kuisha kwa kuwa, inaonekana wazi kuwa matumaini ya kisiasa kwa siku zijazo kati ya Mbowe na Zitto yatategemea kwa kiwango kikubwa kuanguka kwa mmoja ama mmoja kuondoka katika Chadema na kwenda chama kingine.
Kwa sasa baada ya Mbowe kushika nafasi ya juu, mbinu inayotumika ni ile ya kuwanyofoa wafuasi wa Zitto mmoja mmoja kwa nia ya kumdhohofisha. Mbinu kama hii iliwahi kutumika pia kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Hayati Wangwe. Chadema kinatajwa kuwa Chama cha Maendeleo ya Wachaga kwa kirefu kuwa ni Chaga Development Manifesto (CHADEMA).
Wachambuzi wa siasa nchini, wanabaini kuwa kwa kutazama sera na mapenzi ya
wanachama wa Chadema hasa walioko chini, wanaamini kuwa uendeshaji wa chama
chao ngazi ya taifa una dosari. Dosari hizi hasa zipo katika matumizi ya fedha
ambapo viongozi wa juu wanaelezwa kujilipa fedha za ruzuku kutoka serikalini
wakidai wanafidia madeni waliyotumia wakati wa kampeni.
Maoni
Jina
Barua Pepe