TAZARA YANYOFOLEWA
Na Patrick Mwillongo
KUNA kila dalili kuwa wakubwa wanaoendesha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), sasa wameamua kugawana mbao za jahazi walilopanda.
Baada ya jana gazeti hili kuripoti hujuma zinazohusiana na uuzaji wa mabehewa 10 na viberenge vya mamlaka hiyo kinyemela, sasa siri nzito zimevuja kuwa kila mwenye nafasi ndani ya TAZARA anachukua chake mapema.
“Ninachoweza kusema, sasa imebakia kuuza wafanyakazi. Kama ni jahazi litazama muda wowote. Wakubwa wameamua kugawana mbao bila kujali kuwa mtumbwi uko baharini. Si siri kuwa tutazama.
“Hicho alichoelezwa Waziri (Shukuru) Dk. Kawambwa ni cha mtoto. Wakubwa wanajua ingawa walimpiga chenga. Ghala kubwa kuliko yote la TAZARA lililokuwa Mbeya nalo tayari limeuzwa,” alisema mtoa habari wetu.
Wakizungumza na gazeti hili wafanyakazi hao walisema baadhi ya viongozi wa mamlaka hiyo wamechukua jukumu la kuuza maghala kwa mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia bila ya kuwapo kwa taarifa yeyote kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
“Unajua TAZARA kwa sasa imekuwa ni kama mali ambayo haina mwenyewe, kwani watu wanajifanyia mambo bila ya kufuata kanuni, taratibu na miongozo ya mamlaka, hali ambayo inazidi kuididimiza na kufanya kusiwe na mipango ya wakati ujao,” alisema mfanyakazi mwingine.
“Nani asiyejua kuwa Stesheni ya Mbeya hapo awali ilikuwa ni sawa na Bandari ya Nchi Kavu? Mizigo mingi ya kuelekea katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilikuwa inapitia hapa, lakini kama viongozi hawa wameiuza basi kutakuwa hamna huduma hiyo tena,” alionya mfanyakazi mwingine.
Alisema ukiachana na hilo la kuuza mabehewa, viberenge na kuuza maghala ya kuhifadhia bidhaa zilizokuwa zikingoja kusafirishwa kwenda katika nchi za kusini mwa Afrika, pia baadhi ya vigogo wa mamlaka hiyo wamekodisha mabehewa ya Shirika la Reli la Zambia (RSZ), ambayo yanalipiwa gharama kubwa.
“Sasa hii akili gani kuuza mabehewa kwa mtu binafsi na kisha kwenda kukodi mengine kwa gharama kubwa kutoka nchini Zambia? Hii yote inatokana na muundo mbovu wa uongozi wa menejimenti tangu hapo awali wakati reli ilipokuwa ikiasisiwa,” alisema.
Alisema mfumo wa viongozi wakuu ndani ya TAZARA bado upo kisiasa zaidi kama sera za uanzishwaji wa mamlaka hiyo zilivyo na kuongeza kuwa hata baadhi ya malipo yanayokatwa kwa wafanyakazi wa TAZARA kwa muda mrefu hayafikishwi katika mahala husika. Kibaya zaidi wamefikia hatua ya kulipwa kwa mafungu mishahara yao.
Alisema inawezekana hata Waziri wa Miundombinu hapewi taarifa za utendaji wa Mamlaka hiyo badala yake hata Bodi ya Mamlaka imekuwa haikutani kwa wakati, hali inayochangia kutotolewa kwa baadhi ya maamuzi ambayo yangeonyesha mustakabali wa mamlaka.
“Kwa mfano kuna mabehewa mengi sana kandokando mwa reli ambayo yalipata ajali kama yangenyanyuliwa basi kulikuwa hakuna ulazima wa Tazara kuwa na upunguzfu wa mabehewa mpaka kufikia hatua ya kukodi mengine kutoka nchini Zambia kwani yaliyopata ajali yangefanyiwa ukarabati mdogo tu na kutumika,” alisema mfanyakazi mwingine kwa uchungu.
Katika hatua nyingine wafanyakazi hao walimtaka Waziri wa Miundombinu kufanya ziara ya kutembelea stesheni za mamlaka hiyo aone kero wanazopata watumishi wa mamlaka hiyo na wanavyofanya kazi katika mazingira magumu.
“Huwezi amini TAZARA tunafanya kazi kama waganga wa kienyeji kwani mfumo wetu wa mawasiliano umekwama na hivyo kupelekea mawasiliano ya uendeshaji wa garimoshi baina ya kituo na kituo kuwa mbaya. Na hii haina mfano duniani kote katika mifumo ya reli inaweza kuchangia ajali mbaya ya treni,” alionya.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutokea mjini Beijing China, Waziri wa Miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa, alikiri kuwapo kwa taarifa hizo za uuzwaji wa maghala na ukodishwaji wa mabehewa na kuongeza kuwa ameitaka menejimenti ya TAZARA kumpatia maelezo ya kina kuhusiana na masuala hayo.
Pia ameahidi kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuwa walitenda kinyume na kanuni na taratibu za serikali.
Alisema mamlaka hiyo ina matatizo makubwa kiasi cha kufikia kukaa pamoja na wabia wenza kutoka nchini China kuangalia namna ya kuboresha ufanisi wa mamlaka hiyo.
“Ni kweli kumekuwa na mapungufu makubwa mno katika utendaji kazi wa menejimenti ya TAZARA na tunachokifanya kwa sasa ni kutaka mfumo wa uongozi wa ndani kubadilishwa ili kuwapo na watu wenye uwezo wa kuongoza mamlaka hii,” alisema Dk. Kawambwa.
Dk. Kwambwa aliitaka menejimenti ya TAZARA kufanya kazi kwa uhakika na ufanisi mkubwa kuboresha na kuongeza tija kwa maslahi ya mamlaka hiyo na wananchi wa pande zote mbili za Tanzania na Zambia
Kawambwa alisema TAZARA kwa sasa iko katika mchakato wa kuondolewa katika mfumo wa serikali na kubinafsishwa na, hivyo aliwataka wafanyakazi kuwa na subira katika kipindi hiki cha mpito.
Alisema kuingia katika ubinafsishaji wa TAZARA Serikali imekuwa makini mno kwani imechukua tahadhari kuepusha mapungufu yaliyotokea katika ubinafsishaji na mkataba wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kampuni ya RITES ya nchini India.
“Tutahakisha kuwa tunakuwa makini katika kuingia mkataba na kampuni itakayotaka kuendesha TAZARA kwani tunataka sura ya mabadiliko katika uendeshaji wa Mamlaka hii. Tumejifunza vitu vingi sana katika mkataba wa awali tulioingia na wenzetu wa RITES katika uendeshaji wa kampuni ya Reli nchini,” alisema Kawambwa.
Alisema katika kuelekea kwenye mchakato huo, TAZARA pia itasaini mkataba na Serikali ya Watu wa China kwa ajili ya kununua vichwa vipya vya treni. Aliitaka Menejimenti ya TAZARA kutumia mapato yanayopatikana kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na ununuzi wa vifaa.
Maoni
Jina
Barua Pepe