HOTELI ALIYOFUNGUA KIKWETE YAVUNJWA
Na Eliya Mbonea, Arusha

SAA 48 tu tangu Rais Jakaya Kikwete azindue Hoteli ya Kitalii ya Snow Crest huko Ngulelo mjini Arusha, Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) wameivunja.

Jana saa 11.30 asubuhi, tingatinga la wakala hao lilifika hotelini hapo pembeni ya barabara ya Arusha – Moshi na kuvunja ukuta wa mbele na geti la hoteli kwa madai umejengwa ndani ya hifadhi ya barabara.

Hoteli hiyo ilizinduliwa Ijumaa iliyopita na Rais aliyeonyesha kuridhishwa na ramani ya hoteli hiyo pamoja na ujenzi wake.

Rais, katika mazungumzo hotelini hapo, alionyesha kukerwa na tabia ya wafanyakazi wazawa wanaoendekeza wizi na udokozi na kuwaogopesha wamiliki wa hoteli hivyo kuamua kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Kikwete pia aliwapongeza wamiliki wa hoteli hiyo yenye vyumba 83.

MTANZANIA likiwa katika eneo la tukio lilishuhudia ukuta ambao awali ulikuwa umenakishiwa kwa taa na kupambwa kwa vimulimuli vya kukaribisha wageni hasa kipindi hiki cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka ukiwa umepondwapondwa na katapila la TANROAD na kuharibu mandhari nzima ya eneo hilo.

Baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo walionekana wakiokota mabaki ya tofali za ukuta huo.

Mkurugenzi wa Hoteli hiyo, William Tarimo alisema kitendo hicho kinaonyesha kuwapo kwa chuki za kibiashara na kushangaa kwa nini ukuta huo uvunjwe wakati wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa bado wamepumzika.

“Ni chuki, ukitembea kutoka hapa hadi KIA utakuta nyumba nyingi tu zimesogea barabarani, lakini wametuoana sisi tu.
 
“Tulikuwa tumekubaliana kuwa kilichotakiwa kutolewa ni grill na si uharibifu wa eneo la kuegesha magari kama hivi. Tulikubaliana kuwa hiki tulichokiweka ni kwa muda tu,” alisema Tarimo.

Alisema uvunjaji huo umeharibu miundombinu kadhaa ya hoteli hiyo kama simu na umeme.

“Hizi ni chuki za kibiashara. Kama sisi wawekezaji wa ndani tunafanyiwa hivi hii ni hatari sana,” alisema Tarimo

Alisema ofisa wa TANROADS alishirikishwa wakati wa ujenzi wa uzio huo wa muda na hakukuwa na haja ya kubomoa vile na kuipa hasara ya mamilioni ya fedha hoteli hiyo.

Diwani wa Kata ya Baraa, Paul Laizer aliyefika eneo la tukio alisema ameshangazwa na uamuzi wa haraka haraka wa kuvunja uzio huo siku mbili tu tangu Rais aizindue.

“Si kitendo cha kiungwana kabisa. Ilipaswa kuwepo kwa mawasiliano ya kiungwana si namna hii. Wangejaribu hata kuheshimu uwepo wa raia wa nje au basi wangemuheshimu Rais,” alisema Diwani huyo.

 
Meneja wa TANROAD Mkoa wa Arusha, Desdatus Kakoko akizungumza na waandishi wa habari juu ya uvunjaji huo alisema tayari kulikuwapo maelewano kati yake na mmiliki wa hoteli hiyo kuvunja ukuta na geti hilo mara baada ya ujenzi kukamilika.

“Yeye alitaka muda zaidi lakini sisi tayari tulishakubaliana naye kuwa atakapomaliza ujenzi tutakwenda kuondoa au aondoe mwenyewe, lakini badaye aliomba iwe baada ya ufunguzi, tukakubali. Kwa hiyo kilichofanyika hapo ni kutofautiana kwa muda hakuna jambo jipya,” alisema.

Alisema TANROAD inatambua umuhimu na thamani ya hoteli hiyo kwa nchi na Watanzania wote. Bosi huyo alipinga dhana kuwa uvunjaji wa hoteli hiyo ni dharau kwa Rais.

.

Maoni

Jina

Barua Pepe

 


Logo Logo
||Mtanzania|| Bingwa|| Rai|| Dimba|| The African||
TANGAZA NASI
Click to View National Business Directory Details
Home
Maoni ya Mhariri
Habari za Kitaifa
Habari za Kimataifa
Wazo Binafsi
Makala na Barua
Udhamini
Biashara
Elimu na Jamii
Michezo
Burudani
Directory 2010
Wasiliana Nasi