AHSANTE RAIS KIKWETE
JANA Rais Jakaya Kikwete ametimiza miaka minne ofisini tangu ashike madaraka ya urais. Kipindi cha miaka minne kimekuwa na masuala mengi mazito; mazuri na mabaya. Sura mbaya ni kwamba ndani ya miaka minne, amelazimika kuunda Serikali mara mbili.
Ameunda Serikali mara mbili baada ya Baraza la Mawaziri la Kwanza kuvunjika kutokana na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwajibika akajiuzulu baada ya kashfa ya Richmond. Katiba iko wazi kuwa Waziri Mkuu akijiuzulu, Baraza la Mawaziri linavunjwa. Huu ulikuwa mtihani kwa Kikwete.
Ukiakcha hilo, Rais Kikwete ameifanyia nchi masuala mengi mazuri. Wapo watu wenye macho, lakini kwa makusudi wanaamua kuyafumba na kujifanya hawaoni. Shule za sekondari zikitumika kupima utandaji wake, basi tunadhani hakuna atakayemsahau Rais Kikwete.
Enzi hizo wakati Lowassa anasimamia ujenzi wa shule za kata, wapo waliolalamika kuwa anawaumiza. Tukumbuke Lowassa alikuwa anafanya kazi halali aliyotumwa na Rais Kikwete. Leo watoto wengi wanashinda na kuingia sekondari, tunafurahia matunda. Hatusikii wakijitokeza watu kumpongeza Rais kwa mafanikio haya!
Katika elimu ya juu, yapo mengi ameyafanya Kikwete, lakini itoshe tu kutaja Chuo Kikuu cha Dodoma. Inawezekana baadhi ya watu hawajafika kukiona chuo hiki, ila kama taifa, ameipa heshima elimu ya juu nchini. Chuo hiki ni cha kupigiwa mfano barani Afrika.
Wakati Kikwete anaingia madarakani, ujambazi ulikuwa wa kutisha. Alisema bila kuuma midomo kuwa angepambana na majambazi na kuhakikisha anawashinda. Hali ikoje leo? Ndiyo, wapo wadokozi, lakini tulipofikia hata magari ya abiria yameanza tena kutembea usiku.
Mungu apishe mbali, lakini sikukuu hii inakaribika hatujasikia gari limetekwa, wala benki au kituo cha mafuta kimevamiwa na kupora fedha, matukio yaliyokwishageuka sehemu ya maisha ya Watanzania miaka mitano iliyopita. Sisi tunasema, mwenye macho haambiwi tazama, takwimu zinathibitisha uwezo wa Kikwete.
Mwisho, Kikwete ameruhusu wananchi kutoa mawazo yao bila woga. Kwa bahati mbaya wapo watu wanaotumia vibaya uhuru huu. Wameutumia kuwachimba wasaidizi wa Kikwete, kwa kiwango fulani wakafanikiwa kabla jamii haijawashitukia. Tumetishika zaidi, tulipoona watu wale wale, wamemgeukia Rais Kikwete wakitaka eti asigombee tena urais mwaka 2010. Hili Watanzania tusiliunge mkono. Tuwapuuze. Asante Rais Kikwete.